Mshambuliaji wa Timu ya JKT Tanzania, Sixtus Sabilo, ni mmoja wa wachezaji 26 waliochaguliwa kuunda Timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni kwa ajili ya mashindano ya Afrika Ukanda wa Kusini ‘COSAFA’.
Mshambuliaji huyo ambaye ndiye tegemeo la JKT Tanzania, ametangazwa kuwa mmoja wa wataokaunda kikosi hicho kwa ajili ya mashindano hayo ya mwaka huu.
Mbali na mchezaji huyo, wachezaji wengine walioteuliwa wanaochezea Ligi Kuu Tanzania Bara ni Ismail Gambo wa KMC na Awadh Salum wa Mtibwa Sugar.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Boniface Pawasa, amesema ameita kikosi hicho kwa ajili ya kufanya mazoezi na maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo ambayo tarehe ya kuanza na nchi mwenyeji vitatangazwa baadae na wahusika.
Ametangaza wachezaji watakaounda kikosi hicho, mbali na Sabilo wengine ni Ibrahim Abdallah, Yahaya Tumbo na Juma Sultan kutoka Vingunguti Kwanza, Derick Kanyana na Andrew Daniel (Kijitonyama FC), Haji Ally (KMIM ya Zanzibar), Kelvin Mosha, Jaruph Juma na Goodluck Gama kutoka Friends of Mkwajuni.
Wengine waliotajwa ni Abdulkadir Ally kutoka Zanzibar, Jamal Salehe (Mlandege ya Zanzibar) na Abdulrahim Bausi (Uhamiaji ya Zanzibar).
Beki huyo wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars, pia amewaita kikosini Nicholaus Mbando wa Warriors, Patrick Athanas (Msasani Mabingwa), Adil Nassor (Mburahati FC), Abdilah Mohamed (Ilala FC).
Thobias Francis wa Zanzibar, Jume Haji (Kisa FC), Sadiq Salim (Green Warriors) na Mtoro Nassor wa Zanzibar.