Kikosi cha Mabingwa wa Soka nchini Algeria CR Belouizdad kitaondoka mjini Algiers kwa usafiri wa ndege binafsi kuelekea jijini Dar es salaam, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Jumamosi (Februari 24) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Taarifa iliyotolewa na CR Belouizdad kupitia vyanzo vyake vya habari vimeeleza kuwa, Miamba hiyo itaondoka leo Jumanne (Februari 20), na imekubaliana kuwahi jijini Dar es salaam, ili kuzoea hali ya hewa.

Kwa sasa jijini Dar es salaam kuna hali ya hewa ya Joto kali linalokadiriwa kufikia nyuzi joto 27-33 na unyevunyevu karibu 80% – 90%, hivyo Uongozi wa CR Belouizdad unaamini kwa kipindi cha siku kadhaa kabla ya mchezo huo kikosi chao kitaweza kuzoea mazingira ya jiji hilo.

Mchezo huo utakaochezeshwa na Mwamuzi kutoka nchini Mali Boubou Traore, umepangwa kuanza majira ya saa moja usiku katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Katika msimamo wa Kundi D, Young Africans inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tano sawa na CR Belouizdad ambaye ipo nafasi ya pili, Medeama FC ipo nafasi ya nne kwa kukusanya pointi nne na Al Ahly inaongoza kundi hilo ikiwa na alama sita.

Tanzania mwenyeji Mkutano Mkuu Michezo ya Majeshi Duniani
Taifa Stars yaruka kihunzi AFCON 2025