Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani – CISM, unaotarajia kufanyika nchini Mei 13, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo Mkuu wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani, Meja Jenerali Francis Mbindi, ambaye amesema Tanzania itakuwa wenyeji na muaandaaji wa mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 12 – Mei 19, 2024.
Amesema, “hii itakuwa ni wa mara ya 79 tangu kuanza kufanyika kwa mikutano kama hii. Na mwaka 1991 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa tukio hili jijini Arusha, na tunategemea kuwa na wageni 300 watakaoshiriki katika Mkutano huu.”
Mbindi meongeza kuwa, “lengo la baraza hili ni kutumia shughuli za michezo na utimamu wa mwili kama njia ya kueneza amani duniani, tunu za baraza kuhamasisha mshikamano, urafiki, heshima, usawa, uadilifu na ushupavu Duniani.”
Hata hivyo, amesema Mgeni rasmi siku ya ufunguzi Mei 13, 2024 anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na siku ya kufunga Mei 17, 2024 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa