Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imesema kuanzia Januari hadi Desemba 2023 imekamata kilogramu 1,965,340.52 za aina mbalimbali za Dawa za kulevya.
Kauli hiyo imetolewa mbele ya Waandishi wa habari hii leo Februari 29, 2023 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na uratibu), Jenista Mhagama wakati akielezea mafanikio ya Serikali katika mapambano dhidi ya Dawa za kulevya kwa mwaka 2023.
Amesema, Watuhumiwa 10,522 ambao kati yao wanaume ni 9,701 na wananwake ni 821 walikamatwa kuhusika na dawa hizo, huku jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa.
“Kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilichokamatwa katika kipindi cha miaka 11.”
“Na Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria,” alibainisha Mhagama.
Hata hivyo, amesema Tafiti zinaonesha matumizi ya dawa za kulevya yanaanza katika umri mdogo kati ya miaka 10 na 12 na kwamba Serikali inaendelea kutoa elimu kwenye makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya viongozi wa dini, wa kimila, Waandishi wa Habari, Vyombo vya ulinzi na usalama, Maafisa forodha na wakulima.
“Pia katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi na mirungi Vilevile, elimu ya dawa za kulevya imeendelea kutolewa kupita vyombo vya habari, makongamano na maonesho ya kitaifa na kimataifa,” aliongeza Mhagama.