Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewatahadharisha viongozi wote wanaotokana na CCM wasiotimiza wajibu wao kuwatumikia watu, kwa kadri ya matarajio ya Chama na wananchi, na badala yake wanatanguliza maslahi yao binafsi, siku zao zinahesabika, kwani CCM haiwezi kuwavumilia.
Dkt. Nchimbi amesema kuwa viongozi wote wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi wanatarajiwa kuwa watumishi wa wananchi waliowachagua, wakiwatumikia kwa nguvu zao zote, wakiweka maslahi ya umma na Watanzania mbele wakati wote, kabla ya masuala yao binafsi.
Ameyasema hayo alipokuwa akisisitiza namna bora ya kumuenzi Hayati Balozi (mst) Deodorus Buberwa Kamala, kupitia salaam za pole na rambirambi za CCM wakati wa shughuli ya kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, iliyofanyika leo Februari 20, 2024, kijijini kwao Rwamashonga, Kata ya Bwanjai, Jimbo la Nkege, Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.
Mbali ya kutoa salaam za Chama Cha Mapinduzi, Balozi Dk. Nchimbi pia aliwasilisha salaam maalum za rambirambi kwa wafiwa na waombolezaji wote na kisha mkono wa pole kwa Familia ya Hayati Dk. Kamala, kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo pia alieleza jinsi Rais Dkt. Samia alivyoguswa na msiba huo.
Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa mojawapo ya uwezo mkubwa wa kiuongozi aliokuwa nao Hayati Dkt. Kamala ni pamoja na saikolojia ya kutafuta suluhisho la changamoto za watu, tangu alipokuwa Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, huku akimwelezea jinsi alivyokuwa muadilifu, aliyechukia rushwa kwa vitendo, kiasi cha kuwa tayari kugharimu na kupoteza Ubunge wa Jimbo la Nkenge, katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, kwa sababu ya hakuwa tayari kupokea fedha kuwasaliti wananchi wa jimbo hilo, aliokuwa anawatetea kwenye changamoto zao.
“Kamala hakuwa mla rushwa. Hili naweza kulisemea kwa kiapo. Hata alipopoteza ubunge, hakuwahi kulalamika. Kwa sababu alijua zile zilikuwa ni hela za udhalimu, hela za usaliti kwa wananchi wake. Watu wa namna hii lazima tuwaenzi vizuri kwa kutambua mchango wao mkubwa. Hongereni sana Misenyi kwa kuwa na Mwana wa Afrika wa namna hii. Mjisikie fahari sana. Nimefurahi hapa kusikia Mwenyekiti wa Halmashauri na Mbunge wa sasa (Jimbo la Nkenge) walivyoelezea mambo aliyofanya Dk. Kamala na walivyo tayari kuyaendeleza na kufanya zaidi.
“Viongozi tunayo mengi ya kujifunza kwa watu kama Dk. Kamala. Vijana mnayo mengi ya kujifunza kwa Dk. Kamala. Hasa jinsi ya kutimiza wajibu kwa kuwatumikia wananchi. Kuweka maslahi ya nchi na kuwa na msimamo thabiti bila kigugumizi kwenye maslahi ya nchi. Na sisi Chama cha Mapinduzi wajibu wetu tutawatetea na kuwalinda viongozi wanaotumikia wananchi na kutimiza wajibu wao.
“Wale viongozi wachache ambao bado wanasuasua katika kutumikia wananchi, tunawataka wakaze buti. Wale wachache wanaotanguliza maslahi yao binafsi mbele, ambao hawatimizi wajibu wao kuwatumikia wananchi, siku zao zinahesabika. Tunatakiwa kuwatumikia wananchi kwa nguvu zetu zote,” amesema Balozi Dkt. Nchimbi.
“Dkt. Kamala alikuwa na msimamo usioyumba kusimamia maslahi ya nchi. Kwenye vikao vya kimataifa, linapokuja suala la kutetea maslahi ya Tanzania, Kamala hakuwa na kigugumizi hata kidogo. Alikuwa na uwezo wa kusema bila kuangalia anaowakatalia wanatoka mataifa gani na watamfikiraije, alikuwa hamwangalii mtu usoni anatokea wapi. Alikuwa na madhaifu yake kama binadamu lakini yanazidiwa na uwezo na nguvu.”
Hayati Dkt. Deodorus Buberwa Kamala, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Nkenge kwa nyakati mbili tofauti, kabla ya kuwa Naibu Waziri wa Afrika Mashariki na Waziri wa Afrika Mashariki na kisha Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Nchi ya Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya, mjini Brussels, alifariki Februari 12, 2024 na alizikwa jana Jumanne, Februari 20, 2024, kijijini kwake, Rwamashonga, Bwanjai.