Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabit Zacharia ‘Zaka Zakazi’, amesema mazingira ya hali ya hewa ‘Jua Kali’ ni moja kati ya sababu ya kushindwa kuondoka na alama tatu katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Azam FC juzi Jumatatu (Februari 19) ilishindwa kufurukuta mbele ya Tabora United na kuambulia matokeo ya suluhu, na kuifanya timu hiyo ya jijini Dar es salaam kukwea hadi nafasi ya pili kwa alama 36 sawa na Simba SC, lakini ikikaa juu kwa mabao mengi ya kufunga, ikiwa imezidi pia mchezo mmoja.
“Hatukutegemea kupata matokeo ya namna ile, lakini tulikuwa tunajua Tabora United wana kikosi kizuri, malengo yetu tulijiandaa kushinda, lakini kwa tahadhari kubwa kwa sababu tulijua tunakwenda kukabiliana na timu bora ambayo haipo kwenye nafasi nzuri na unapokutana na timu hii ni hatari sana,”
“Tumeathirika na hali ya uwanja haukuwa rafiki, lakini mechi nyingi sisi Azam FC msimu huu tulikuwa tunacheza usiku, tulicheza mchana jua lilikuwa kali sana lilituathiri pia kwa asilimia 100,” amesema Zaka Zakazi.
Kocha Youssouph Dabo, amesema baadhi ya wachezaji wake hawakuwa sawa kwenye mchezo huo hasa kwenye maamuzi ya mwisho, lakini pia akilia na majeruhi kikosini mwake ambao ni Prince Dube na Gibrill Sillah.
Kingine ni baadhiya wachezaji wetu wametoka kwenye majeraha, hawajakuwa. Ilikuwa ngumu kwetu, baadhi ya wachezaji wetu hawakuwa sawa, hatukuwa na maamuzi mwishoni. Inabidi mechi zetu zote tucheze sawa na zingine, tunajisahau kwenye baadhi ya mechi tuna mechi nyingi mbele lazima tubadilike,” amesema Dabo.
Wakati Azam ikifikisha alama 36, Tabora United ipo nafasi ya 13 na alama zake 17.