Kikosi cha Simba SC huenda kikabwa na mambo mawili tofauti kuelekea mchezo wake wa Mzunguuko watano wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Asec Mimosas.

Simba SC itacheza mchezo huo keshokutwa Ijumaa (Februari 23) katika Uwanja wa Felix Houphouet Bounie mjini Abidjan-Ivory Coast, huku ikihitaji ushindi ili kujiweka kaatika mazingira mazuri ya kufuzu Robo Fainali.

Endapo Simba SC itashinda kwenye mchezo huo, itakuwa imeweka hai hesabu zake za kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikijua wazi Asec Mimosas inataka heshima tu, kumaliza kinara wa Kundi B ikiwa imeshafuzu baada ya kufikisha pointi 10.

Hata hivyo, mapema tu hesabu zimeanza kuibeba Simba SC nje ya uwanja baada ya wekundu hao kuwa tayari kimchezo na imecheza mechi tano za ligi kuanzia Februari 3, 2024, iliposhinda ugenini dhidi ya Mashujaa FC ya mjini Kigoma.

 

SIMBA HATARI UGENINI:

Simba imeshinda mechi zote nne ugenini na kuvuna jumla ya pointi 12, kisha ikalazimishwa sare nyumbani dhidi ya Azam FC na kufanya timu hiyo kukusanya alama 13 ndani ya mechi tano.

Iko hivi, mechi hizo zitakuwa zimewajenga Simba kwa ajili ya mechi yao na ASEC ambao tangu mwaka huu uanze haijacheza mechi yoyote ya mashindano ingawa imekuwa ikicheza mechi kadhaa za kirafiki.

Mara ya mwisho ASEC kucheza mechi ya mashindano ni Desemba 30 ikishinda nyumbani bao 1-0 dhidi ya Stade d’Abidjan la mkwaju wa Penati iliyopigwa na kiungo Serge Pokou na ndiye staa wa kuchungwa na Simba.

 

SIMBA BORA:

ASEC ikiangalia hata msimamo wa ligi ya hapa itashtuka kwani Simba SC ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36, baada ya kucheza mechi l6, ambazo ni alama 10 zaidi ya zile ambazo inazo wapinzani wao waliopo nafasi ya nne na pointi 26 baada ya kucheza mechi 15.

Simba SC pia ina safu ya ushambuliaji inayofunga mabao kwani kwenye ligi imeshafunga mabao 31 huku ikiruhusu 14, wakati wenyeji wao hao mpaka ligi yao inasimama kupisha Fainali za Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’, zilizofanyika nchini kwao ilikuwa imefunga mabao 20.

 

PIGO KUBWA KWAO:

Pigo kubwa kwa ASEC ni mshambuliaji wao kinara wa mabao Sankara Karamoko ambaye alishafunga mabao sita kwenye Ligi ya Mabingwa hatakuwa sehemu ya mchezo huo kwa mara ya kwanza, baada ya kuuzwa kwenda klabu ya Wolfsberger AC ya Austria kwenye usajili wa dirisha dogo, ndiye aliyetoa asisti wakati Simba SC ikilazimishwa sare nyumbani na miamba hiyo kutoka Afrika Magharibi.

Polisi wafanikiwa kudhibiti wizi kupitia Bodaboda Moro
Dube akitamani kiatu cha dhaharu Ligi Kuu