Lydia Mollel – Morogoro. 

Kutokana na baadhi ya mitaa ya Morogoro, kuwa kero katika kipindi cha nyuma kufuatia uhalifu wa wizi wa mikoba na simu kwa kutumia Pikipiki kushika kasi, hali inadaiwa kupungua kama si kuisha kabisa baada ya mbinu za Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na waendesha Pikipiki Wastaarabu kuzaa matunda.

Mbali na Operesheni mbalimbali za kukamata wahalifu wa aina hii, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro kupitia Polisi Kata, limesema lilikuja na mbinu ya kutoa elimu kwa kila kijiwe cha bodaboda na kuwataka  kuonyana wao kwa wao na asiyebadilika aripotiwe kituo cha Polisi.

Ushirikiano huo wa bodaboda Wastaarabu na Polisi, umeleta matokeo chanya kwani kila kijiwe kilipewa elimu namna ya kujiongoza kujisimamia pamoja na kujisajili kama kijiwe rasmi jambo ambalo limepelekea bodaboda wahalifu kujichuja dhidi ya waaminifu.

Akiwa katika kijiwe cha Nanenane Kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Magreth Kitundu amesema, mbinu hiyo ya kuongea na bodaboda na kushirikiana nao imekuwa tiba ya uhalifu kwani wahalifu wengi wamekamtwa na kuchukuliwa hatua na sasa Nanenane ni shwari.

Kwa upande wake Polisi Kata wa Kata ya Mkundi, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Amina Manumbu amesema, ameanza na kuorodhesha majina ya bodaboda wote katika kila kijiwe na kuwapa utaratibu mzuri wa kupokea wageni, ili vijiwe visije ingiliwa na Wahalifu kwa kujifanya bodaboda wenzao.

Mbinu hii imeenda mpaka kwenye Kata zilizopo Wilayani, ikiwemo Kata ya Mbingu, Tarafa ya Mngeta  Wilaya ya Kilombero ambapo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Patrick Stanley, amesema kwa Kata yake  bodaboda wote wameshapatiwa elimu na wamebadilika anachokifanya kwa sasa ni kupita na kuwakumbusha lakini pia kuendeleza umoja baina yao.

Kata nyingine ambazo elimu hii inaendelea kutolewa ni pamoja na  Nawenge Tarafa ya Vigoi Wilaya ya Ulanga chini ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Hussein pamoja na Chisano Tarafa ya Mlimba chini ya Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mcha.

Polisi wafanikiwa kudhibiti vurugu bila uharibifu Babati
Mzani waipendelea Simba Ivory Coast