Timu ya taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ inaendelea kujifua kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni kujiandaa na mechi ya raundi ya tatu kufuzu michuano ya Olimpiki utakaopigwa kesho ljumaa (Februari 23) kwenye Azam Complex dhidi ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’.
Jumla ya nyota 24 wanaocheza Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na wale wanaocheza soka la kulipwa nje watakuwa na kibarua kigumu mbele ya ‘Banyana Banyana’, baada ya awali kuzing’oa Congo na Botswana kwenye mechi za raundi ya kwanza na ya pili.
Hii ni mara ya nne kwa timu hizo kukutana na Rekodi zinaonyesha Twiga haijawahi kufurukuta mbele ya wapinzani wao, hivyo kesho watakuwa na kazi ya kufuta unyonge na kujiweka pazuri kwenda Olimpiki.
Mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana mwaka 2006, Stars ilichapwa 4-0 kisha marudiano ikafungwa 3-0, huku 2010 ikipoteza tena kwa 2-1.