Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Thabo Senong amesema kukosekana nyota wake wawili kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma na beki wa kati Abdulmajjid Mangalo, kimewapa mtihani kwenye mechi zao za hivi karibuni.
Kagoma na Mangalo waliokuwa muhimili wa kikosi hicho katika eneo la ulinzi na kiungo, wanasumbuliwa na majeraha na mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Januari 10 katika Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba SC na kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amesema ni pengo kwenye kikosi hicho kwa hivi karibuni.
Singida imecheza mechi mbili za Ligi Kuu bila nyota hao wakipoteza yote kwa kulala 1-0 mbele ya Kagera Sugar kisha kulazwa 3-1 na Tanzania Prisons, japo mwanzoni mwa juma hili ilishinda mabao 2-0 dhidi ya FGA Talent katika mechi ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kocha Senong amesema kukosekana kwa nyota hao imeifanya timu hiyo kukosa uongozi katika eneo la ulinzi na kiungo hadi kujikuta wakichechemea katika mechi zilizopita.
Msauzi huyo amesema kwamba licha ya kukosekana kwao lakini kikosi chake kinazidi kuimarika na kufanyia kazi upungufu, huku akiwapa nafasi wachezaji wengine ili kuhakikisha malengo yao yanatimia.
“Kagoma na Mangalo bado ni majeruhi na mchango wao unakosekana katika eneo la kiungo na ulinzi kuwa na kiongozi lakini timu yetu ya madktari inafanya kazi natumaini watarejea hivi karibuni,” alisema kocha huyo, huku Ofisa Habari wa timu hiyo, Hussein Massanza akiongeza, kikosi chao kina kazi kubwa ya kuhakikisha kinapata ushindi kwenye michezo miwili inayofuata dhidi ya Tabora United na Azam FC ili kurejesha imani kwa mashabiki wao.
“Tunaendelea kujipanga vizuri, ni lazima turudishe imani kwa mashabiki wetu na ili kuwapa raha lazima timu ipate ushindi katika mechi zijazo na tutafanya hivyo,” ametamba Massanza.