Ratiba ngumu ya kucheza bila wachezaji kupata mapumziko ya kutosha yamemfanya kocha mkuu wa Geita Gold, Denis Kitambi kushindwa kujizuia kwa kusema imechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kushindwa kupata matokeo mazuri ya Ligi Kuu Bara inayoendelea.
Geita imecheza mechi tatu mfululizo ndani ya siku tisa ikianza dhidi ya Simba SC Februari 12, jijini Mwanza, kisha ikasafiri kwa Kilometa 853 kuifuata Azam FC jijini Dar es Salaam Februari 16 kabla ya kurudia tena nyumbani mjini Geita kuivaa Ihefu mchezo uliopigwa Februari 19 na zote ilipoteza.
Katika mechi hizo Geita ililala 1-0 mbele ya Simba SC, kisha kupigwa 2-1 na Azam FC kisha kulala tena 2-1 mbele ya Ihefu na kuifanya kuruhusu mabao matano na yenyewe kufunga mawili tu na kushika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 16.
Kitambi amesema timu yake inakutana na wakati mgumu kutokana na namna ambavyo ratiba imekaa, ambapo kila baada ya siku mbili inatakiwa kucheza wakati huo miundombinu ya usafiri ikiwa siyo rafiki kwani wao wanatumia basi.
Akitolea mfano mchezo wao wa nyumbani dhidi ya Ihefu, amesema ilitokana na wachezaji wake kukosa muda wa kutosha kujiandaa na kupumzika akisema uchovu uliwagharimu.
“Ratiba ndio imetoka inabidi twende nayo hivyo hivyo kikubwa tutajitahidi kufanya marekebisho ili kuweza kuhimili mikiki mikiki ya Ligi.” amesema Kitambi.
Kuhusu mchezo wa baadae leo Alhamisi (Februari 22) wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Mbeya City utakaopigwa Uwanja wa Nyankumbu, Kitambi amesema wanahitaji ushindi ili kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano hiyo.
“Tunahitaji ushindi japokuwa lazima tuwe makini kwa wapinzani, huu ni mchezo wa mtoano hivyo vijana wanapaswa kucheza kwa tahadhari ili tufuzu hatua inayofuata,” amesema kocha huyo.