Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouf Dabo amewaomba wachezaji wake kuongeza bidii kuendana na ushindani kwenye mbio za ubingwa Ligi Kuu soka Tanzania Bara.
Dabo amesema kwa namna ushindani ulivyo hivi sasa, kila mchezaji anatakiwa kujitoa kwa asilimia 100, kupata uhakika wa Pointi tatu kwenye kila mchezo wa ligi wanaocheza.
“Ligi Kuu Tanzania Bara ni miongoni mwa ligi bora Afrika, ndio maana nimewaomba wachezaji wangu kuongeza bidii katika kila mchezo wa ligi,” amesema Dabo.
Kocha huyo raia wa Senegal amesema anafurahishwa na mapambano ya vijana wake lakini amewataka kuongeza zaidi juhudi kama ilivyo kwa wapinzani wao Young Africans na Simba SC, ili kufikia malengo ambayo wamekusudia kuyafikia mwishoni mwa msimu huu.
Amesema anajivunia ubora wa kikosi chake kinachoundwa na wachezaji wengi wenye vipaji na uzoefu wa mashindano makubwa, hivyo amewataka kutumia kila walichokuwa nacho ili kuhakikisha Azam FC inabeba taji la Ligi Kuu msimu huu.
Amesema mikakati yake kwa sasa ni kushinda kila mchezo wa ligi watakacheza nyumbani na ugenini na anaamini hiyo inaweza kuwa nia rahisi ya kufikia malengo yao.
Azam FC ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikikusanya Pointi 36 sawa na Simba SC lakini Azam ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na ipo mbele kwa mchezo mmoja.