Nyota wa timu ya taifa ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, Aisha Masaka anayekipiga BK Hacken ya Sweden, ataukosa mchezo wa leo Ijumaa (februari 23) dhidi ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ wa kufuzu mashindano ya Olimpiki yatakayofanyika mwakani nchini Ufaransa, baada ya kupata majeraha.
Twiga Stars itamkosa mchezaji huyo muhimu katika mchezo huo wa Mzunguuko watatu utakaochezwa saa l:00 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam, akiwa alifanya kazi kubwa na kuiongoza kushinda mabao 2-0 dhidi ya Botswana, raundi ya pili ya michuano hii.
Akizungumza jijini Dar es salaam Kocha wa timu hiyo, Bakari Shime amesema atamkosa mchezaji huyo baada ya kupata majeraha ya mguu, ingawa mastaa wengine wapo tayari kupeperusha bendera ya taifa.
Shime amesema huu ni mchezo mkubwa kwao na wameshafanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanaibuka na ushindi, ingawa wanafahamu kuhusu ubora wa wapinzani wao.
“Ni mechi kubwa na kila mchezaji angependa kuwa sehemu ya mchezo huu, tunacheza na timu ngumu na tunahitaji ushindi wa nyumbani ili kujiweka pazuri, tumefanya maandalizi ya kutosha na sasa tunasubiri dakika 90,” amesema Shime.
Nyota wa Twiga, Opah Clement amesema wachezaji hawana presha na mechi hiyo na wamejiandaa vya kutosha kuibuka na ushindi.
Tunacheza na wachezaji ambao wana uzoefu mkubwa na soka la Afrika sisi pia tunawafahamu, haitakuwa mechi rahisi kikubwa tunakwenda kupambana na tunaomba mashabiki, wajitokeze kutusapoti,” amesema Opah anayekipiga Besiktas ya Uturuki.
Nahodha wa Banyana, Thembi Kgatlana, amesema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa wanaifahamu Twiga Stars
“Huu ni mchezo muhimu kwetu japo sio rahisi kwa kuwa tupo ugenini na Tanzania tunawajua na wao wanatufahamu vizuri,” amesema Thembi aliyecheza kwenye kikosi hicho kiliposhiriki Olimpiki a mwaka 2016 na 2018 na kutwaa tuzo ya mfungaji na mchezaji bora.
Endapo Twiga itavuka hapo itakutana na mshindi kati Nigeria na Cameroon na ikishinda itakuwa kati ya timu mbili zitakazoiwakilisha Afrika kwenye Michuano ya Olimpiki mwakani.