Nahodha wa kikosi cha Tabora United Said Mbatty amesema kwa sasa wanapitia kipindi kigumu cha upepo wa matokeo yasiyoridhisha licha ya juhudi za wachezaji wanazonesha, akiahidi kurejesha furaha kwa mashabiki watakapoikabili Singida FG.

Tabora United iliyopanda Ligi Kuu msimu huu haijapata ushindi katika mechi tatu mfululizo, ikiwa ni kupoteza moja dhidi ya Simba SC kwa 4-0 kisha sare dhidi ya Namungo na Azam FC.

Timu hiyo ya mjini Tabora inatarajia kuwa nyumbani keshokutwa Jumapili (februari 25) kuwakabili Singida FG ambapo nao hawajapata pointi tatu katika mechi zao tatu za hivi karibuni na kufanya vita kuwa nzito.

Mbatty amesema wachezaji wamekuwa wakionyesha kiwango bora kuipambania timu, lakini wamekumbwa na upepo mbaya wa kutopata matokeo mazuri hasa kufunga mabao.

“Jumapili tunaenda kurejesha upya furaha kwa mashabiki tutakaposhinda dhidi ya Singida FG, tutakuwa makini kufunga mabao ambao yamekuwa tatizo kwetu,” amesema nyota huyo.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Singida Fountain Gate, Thabo Senong amesema baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo kwenye ligi, amesahihisha makosa ya wachezaji hivyo anatarajia ushindi keshokutwa Jumapili (Februari 25).

Amesema mechi zilizopita wachezaji hawakuwa bora kwa kupoteza umakini kwenye kufunga na kuruhusu mabao, hivyo mchezo huo hatarajii makosa hayo.

“Nimewaelekeza wachezaji tunataka nini, mechi zilizopita hatukufanya vizuri tukapoteza pointi tisa, nataka kuona kasi ya mabao na kiwango bora kupambania ushindi,” amesema kocha huyo.

Arsene Wenger aionya Liverpool
Polisi Manyara wazipa ahueni Kaya zenye mahitaji maalum