Kitendo cha Wekundi wa Simba SC kulazimishwa suluhu ugenini kwenye mchezo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast siku ya Ijumaa (Februari 23), kisha Young Africans kushinda mabao 4-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria na kutinga Robo Fainali kupitia Kundi D, kumewachanganya Mashabiki na Wanachama wa Mnyama.

Wanaamini chama lao, lilistahili kuwa la kwanza kutinga hatua hiyo kama ilivyowahi kufanya katika misimu mitatu kati ya mitano iliyopita, lakini kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amewatuliza Mashabiki na Wanachama hao kwa kuwaambia wamwachie yeye kwani anajua anachokifanya na muda si mrefu watafurahi na roho zao.

Simba SC inatarajiwa kuikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mchezo wa mwisho ya Kundi B utakaopigwa mwishoni mwa juma hili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ambapo ushindi wa aina yoyote utaivusha miamba hiyo ya Msimbazi na kuiingia hatua ya Robo Fainali kwa mara ya tano ndani ya misimu sita ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho na nne za Ligi ya Mabingwa.

Kocha Benchikha aliyetwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na CAF Super Cup msimu huu, akiwa na USM Alger ya Algeria, amesema mchezo dhidi ya Jwaneng utakuwa ni zaidi ya fainali kwa Simba, kwani wanahitaji ushindi ili kusonga mbele na tayari amejua namna gani atawamaliza wapinzani wao kutoka Botswana.

Benchikha amesema anautazama mchezo huo kwa jicho jingine na anatarajia kufanya baadhi ya mabadiliko katika kikosi chake ili kutengeneza zaidi mashambulizi tofauti na michezo iliyopita na kwamba mashabiki wasiwe na presha kabisa.

“Mchezo ujayo ni zaidi ya fainali kwetu, tunahitaji ushindi na tayari tumeanza kuandaa namna ya kushinda. Mambo ya ufundi niachiwe mimi na benchi langu la ufundi, tunajua nini tutakifanya, lakini nawaomba mashabiki na wanachama wa klabu yetu kujitokeza kwa wingi zaidi katika mchezo wetu wa mwisho wa kundi B,” amesema Benchikha aliyeiongoza timu hiyo kwenye michezo minne ya hatua ya makundi msimu huu 2023/24 na kuvuna alama tano, ikishinda mara moja na kutoka sare mbili na kupoteza mara moja.

“Ni mchezo wa historia kwa kila mmoja wetu. Tunaamini itawezekana na pia tutawashangaza wengi namna tutakavyoanza na kumaliza mchezo huo,” ameongeza kocha huyo kutoka nchini Algeria.

Simba SC (Tanzania), Jwaneng Galaxy (Botswana) wanafainali wa msimu uliopita wa michuano hiyo, Wydad CA ya Morocco kila mmoja ana nafasi ya kuifuata Asec iliyotangulia Robo Fainali kutoka Kundi B, hivyo kufanya michezo yao ya mwisho itakayopigwa siku na muda mmoja kuwa na utamu wake, kwani wakati Simba SC ikimalizana na Jwaneng jijini Dar es salaam, Wydad itakuwa nyumbani kuikaribisha Asec iliyofuzu tayari kwa kukusanya alama 11 katika michezo mitano ya awali iliyocheza hadi sasa.

Simba SC na Wydad kila moja ana alama sita, lakini matokeo baina yao yanaibea Simba SC kama zitamaliza zikilingana kwa alama, kwa vile matokeo ya jumla timu hizo zilipokutana Simba ilishinda 2-1.

Katika Kundi B, imebaki nafasi moja tu ya kufuzu Robo Fainali baada ya Asec Mimosas yenye alama 11 kujihakikishia kusonga mbele ikiwa kileleni wakati Jwaneng ipo mkiani kwa sasa na alama zake nne tu.

Hata hivyo, rekodi zinaibeba Simba inapocheza Uwanja wa Mkapa kwenye michuzno inayoratibiwa na SHirikisho la SOka Barani Afrika ‘CAF’ kwani tangu msimu wa 2018/2019 katika mashindano yote imecheza jumla ya michezo 24 na kupoteza miwili pekee, ambayo ni ile iliyochapwa 3-1 na hao hao Jwaneng na kuondoshwa katika duru ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2021 kwa bao la ugenini baada ya mchezo wa kwanza kushinda 2-0 ugenini na matokeo ya jumla kuwa (3-3), na ile ya msimu uliopita dhidi ya Raja Casablanca ilipofungwa 3-0.

Wachezaji Shomari Kapombe, Henoc Inonga, Mohamed Hussein, Aishi Manula, Israel Mwenda, Sadio Kanoute, John Bocco, Mzamiru Yassin, na Kenedy Juma ni wachezaji wa Simba SC waliokuwa kwenye kikosi kilichoikabili Jwaneng galaxy mwaka 2021, hivyo mchezo wa mwishoni mwa juma hili utakuwa ni sehemu ya kulipa kisasi kwao.

Tayari kikosi cha Simba SC kimeshaanza safari ya kurejea nyumbani Dar es salaam Tanzania, kikitokea mjini Abidjan nchini Ivory Coast na kitakapowasili moja kwa moja kitaelekea kambini kujiandaa na mtanange dhidi ya Jwaneng Galaxy utakaoamua hatma yao ya kwenda hatua ya robo Fainali ama la.

 

David Moyes: Nina dili mezani
Ahmed Ally: Mo ameisaidia Young Africans