Kocha Mkuu wa West Ham United, David Moyes amethibitisha amepewa ofa ya mkataba mpya ili abaki kwenye kikosi hicho cha London kwa miaka mingine kadhaa.

Kulikuwa na uvumi mwingi kuhusu hali ya maisha ya baadae ya kocha Moyes mwenye umri wa miaka 60, huko West Ham United hasa kutokana na mwenendo wa timu na mkataba wake ukikaribia kufika ukingoni mwisho wa msimu.

Moyes alisherehekea miaka yake minne ya kuwa kocha wa West Ham kwenye ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Arsenal mwishoni mwa Desemba mwaka jana, lakini tangu wakati huo, kocha huyo kutoka nchini Scotland amekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kiwango cha ovyo cha timu yake uwanjani.

West Ham imeshindwa kupata ushindi katika mechi nane za kwanza ilizocheza mwaka huu 2024 kwenye michuano yote, huku ikipoteza mechi tatu za mwisho ilizocheza kwenye Ligi Kuu England kwa jumla ya mabao 11-0, ikimaanisha si kupoteza tu, bali hata kufunga mabao limekuwa tatizo kwao.

Kutokana na hilo, makocha kadhaa walianza kuhusishwa na kibarua hicho cha West Ham United, akiwamo Thomas Tuchel wa Bayern Munich, ambaye itakapofika mwisho wa msimu atafunguliwa mlango wa kutokea huko Allianz Arena.

Moyes amesema: “Nimekuwa kwenye mazungumzo mazuri na wamiliki David Sullivan na Karren Brady. Kuna mkataba mezani na uamuzi wangu mimi tusubiri hadi msimu umalizike”

Moyes aliipa West Ham taji la Europa Conference League msimu uliopita baada ya kuwachapa Fiorentina 2-1 katika mchezo wa fainali na hivyo kunyakua ubingwa wa kwanza wa kombe la Ulaya baada ya miaka 58.

Chini ya Moyes, West Hlam imecheza mechi 245, imeshinda 107 sare 50 na vichapo 88.

Matajiri Saudia wamgeukia Varane
Benchikha awataka Jwaneng Galaxy