Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesera timu yake inahitaji maombi ili kujinasua katika nafasi mbaya iliyopo kwa sasa.
Mtibwa Sugar ilipoteza mchezo mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Coastal Union, hali iliyoendelea kuiweka pabaya timu hiyo ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Kocha Katwila amesema hakutarajia kama wangepoteza mchezo huo kutokana na mazingira mazuri ya maandalizi waliyokuwanayo, hivyo amewataka Mashabiki waendelee kuiombea timu yao katika kipindi hiki kigumu.
“Tunahitaji maombi ya kujitoa kwa wachezaji wangu kwenye huu mzunguko wa pili kwani kuendelea kupoteza mechi kumeendelea kutuweka pabaya kwenye msimamo kitu ambacho siyo kizuri” amesema Katwila.
Kocha huyo amesema yeye na wachezaji wake hawafurahishwi na hali hiyo na wanaendelea kupambana ili kubadili mwenendo wa timu.
Amesema pamoja na wakati mgumu wanaopitia, lakini wataendelea kupambana kuhakikisha wanapata matokeo mazuri na kujiondoa kwenye nafasi waliyopo hivi sasa.
Mtibwa Sugar ipo mkiani mwa msimamo wa ligi hiyo ikikusanya alama nane katika michezo 17 ilyocheza hadi sasa.