Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania “Twiga Stars’, Bakari Shime amesema anaamini wanaenda kukutana na mchezo mgumu wa kuwania kufuzu michuano ya Olimpiki lakini watapambana kutimiza malengo yao.

Twiga Stars inashuka dimbani leo Jumanne (Februari 27) kumenyana na Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ Uwanja wa Mbombela, Afrika Kusini huku wakiwa nyuma kwa mabao 3-0 waliyofungwa kwenye mechi ya awali Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.

Kuingia raundi ya nne ya michuano hiyo ambapo itakutana na mshindi wa mechi kati ya Nigeria na Cameroon, Twiga Stars watahitaji kupata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Banyana Banyana kwenye mchezo wa leo Jumanne (Februari 27).

Shime amesema, bado wana matumaini ya kusonga mbele kwenye mchezo wa kutafuta nafasi ya kufuzu licha ya kuwa wako nyuma lakini tayari wamefanyia kazi upungufu wao kabla ya kuwavaa Banyana Banyana leo.

“Baada ya kuona ubora wa wapinzani wetu na upungufu wao, tutafanyia kazi maeneo hayo mawili ili tuone tunawezaje kutoka nyuma na kurudisha mabao tuliyofungwa ili tupate matokeo mazuri kwenye mchezo huu wa mwisho.

“Bado hatujakata tamaa, vijana wana morali ya hali ya juu kabisa na wanaamini kuwa kilichotokea ni majaliwa ya kimpira na naamini wataendelea na moto walio nao kuhakikisha wanalimiza malengo siku ya mchezo,” amesema Shime

Katika hatua nyingine, Shime amesema ingawa kumekuwa na hali ya hewa tofauti na waliyoizoea Afrika Kusini, ambako kumekuwa kuna joto kali tofauti na ambavyo wamekuwa wakidhani wakati wote lakini wako tayari kwa mchezo.

Young Africans inawaza makubwa Afrika
Waaswa kutopandisha bei ya Vyakula Sokoni