Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Fredy Minziro amesema ushindi walioupata mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Ihefu FC umetokana na wachezaji wake kufuata kikamilifu kile alichowaelekeza kwenye uwanja wa mazoezi.
Katika mchezo huo, Kagera Sugar ikiwa nyumbani Uwanja wa Kaitaba ilibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kupanda hadi nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo wakifikisha alama 21.
Minziro amesema walilazimika kubadili mfumo walioanza nao baada ya wapinzani wao Ihefu FC kuziba njia zote walizopanga kuzitumia na hiyo iliwasaidia kupata bao la ushindi.
“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata kile nilichowaelekeza na kupata ushindi, ulikuwa mchezo mgumu uliohitaji mbinu ili kupata ushindi na ndivyo tulivyofanya, malengo yetu ni kuendelea kufanya vizuri mechi zijazo,” amesema.
Naye Kocha Mkuu wa Ihefu, Mecky Maxime aliwapongeza wapinzari wao Kagera Sugar kwa ushindi huo lakini akaeleza kuvutiwa na ushindani ambao umeoneshwa na timu yake kwenye mchezo huo.
Anthony Martial kuondoka Man Utd
“Hongera kwa Kagera sababu wamepata alama zote tatu lakini niseme mchezo ulikuwa 50-50 yeyote angeweza kushinda, pamoja na kupoteza mchezo huu lakini vijana wangu walicheza vizuri na kutoa upinzani mkubwa, tunakubali matokeo na sasa tunaangalia mechi zijazo,” amesema Maxime.
Kipigo hicho kimeiacha Ihefu FC katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wakiwa na alama zao 19 walizovuna kwenye michezo 17 waliyocheza hadi sasa.