Mahakama ya Mwanzo Wilayani Kalambo, imewahukumu kifungo cha mwaka mmoja jela kila mmoja wakazi saba wa Kijiji cha Kalambo kilichopo Wilayani humo Mkoani Rukwa, baada ya kukutwa na hatia ya kugomea Watoto wao wenye umri kati ya miezi 9 hadi 59 wasipewe chanjo ya ugonjwa wa Surua na Rubela.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoani Rukwa, Shedrack Masija imesema chanjo hiyo ilikuwa ikitolewa na Wizara ya afya katika Kijiji hicho Februari 18, 2024, na washtakiwa waligomea wakidai si maagio ya Mungu na inakinzana na imani ya dini yao ya Kanisa la Watchtower.
Amewataja washtakiwa hao kuwa ni Abiniel Isaya (27), Misheck Simon (28), Isack Simon (26), Yona Simon (30), Efeso Peter (28), Job Simon (36) na Joshua Meshack (40) na walipewa hukumu hiyo Februari 26, 2024 na Mahakimu wa Mahakama Elis Mkama na Suzy Mkinga.
Amesema “kugomea chanjo inayoelekezwa na Serikali ni kufifisha juhudi za kupambana na maradhi hivyo Wananchi wazingatie maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na Serikali na wazitii Mamlaka za Serikali.]