Lydia Mollel, Bagamoyo – Pwani.
Madhara yanayosababishwa na Wanyamapori katika Makazi ya Binadamu maeneo mbalimbali Nchini, yamedaiwa kutokana baadhi ya Watu kuvamia Shoroba za Wanyamapori katika Hifadhi.
Hayo yamesemwa Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani na Afisa Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Isaac Chamba wakati wa mafunzo na Waandishi wa Habari nchini juu ya uhifadhi Wanyamapori
Amesema, “baadhi ya Wananchi wakuwa wakivamia Shoroba za wanyamapori na ndiyo sababu kubwa ya kuwepo kwa migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori ambapo Tanzania kuna zaidi ya shoroba 61 lakini baadhi yake hazionekani kutokana na uvamizi wa wananchi.”
Chamba ameongeza kuwa, Wanyamapori wapatao 108 wameuawa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita (2023), kutokana na kufanya uharibifu katika makazi ya watu huku Simba wapatao 60 wakihamishwa Makazi na kupelekwa kwenye Hifadhi nyingine, ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwa Wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi.
“Wanyamapori hawa waliouawa baada ya kutishia usalama wa wananchi wanaoishi pembezoni mwa maeneo ya hifadhi ambapo Simba,Chui,Tembo na Fisi walionekana kuhatarisha sana usalama hivyo wakalazimika kuuawa,” alisema Chamba.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania – JET, John Chikomo amesema uvamizi wa Shoroba unasababishwa na Wananchi kutokuwa na elimu ambapo aliwataka Waandishi wa Habari za Mazingira kutumia kalamu zao kuielimisha Jamii juu ya suala hilo.
Amesema, katika kukabiliana na changamoto hiyo JET imeamua kutoa mafunzo kwa Eaandishi wa Habari kutoka Vyombo mbalimbali kwa Ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori ili Waandishi hao waweze kutumia kalamu zao kuzielimusha jamii.
Hata hivyo, jumla ya matukio ya migongano kati ya Binadamu na Wanyamapori yanazidi kuongezeka hadi kufikia 2,817 mwaka 2022/2023 kutoka 833 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017 na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini.