Kocha Mkuu wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique, amekiri timu yake inahitaji kujiandaa kwa kuondoka kwa Kylian Mbappe msimu huu wa majira ya joto baada ya kumtoa nahodha huyo wa Ufaransa wakati wa sare na Rennes, Jumapili.

Mbappe alitolewa dakika ya 65 na PSG wakiwa nyuma kwa bao 1-0 nyumbani kwa Rennes na nafasi yake kuchukuliwa na Goncalo Ramos, aliyefunga bao la Penati la kusawazisha dakika ya 97.

“Ni rahisi sana. Hivi karibuni au baadae, inapotokea, lazima tuzoee kucheza bila Kylian,” alisema Enrique alipoulizwa kuhusu uamuzi huo baada ya mchezo huo.

“Ninapotaka kumchezesha, nitafanya nisipomchezesha, hatacheza.”

ESPN iliripoti mapema mwezi huu kwamba Mbappe aliiarifu PSG kuhusu nia yake ya kuondoka wakati mkataba wake utakapomalizika msimu huu wa majira ya joto, na bado yuko kwenye mazungumzo na Real Madrid, ambao wana matumaini ya kumpata mshambuliaji huyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa kocha huyo kuzungumzia kuondoka kwa Mbappe katika klabu hiyo ya Ligue 1, ambako amekaa kwa miaka sita iliyopita.

Katika mkutano na waandishi wa habari Februari 16, mwaka huu, Luis Enrique alisema: “Nitajaribu kumaliza mada hii, sina maoni yoyote ya kutoa.

“Pande zinazohusika bado hazijasema chochote hadharani, Kylian Mbappe hajasema chochote hadharani.

“Wakati pande zote mbili zitakapozungumza, nitatoa maoni yangu.”

Mbappe amefunga mabao 21 katika mechi 21 za Ligue 1 msimu huu, pamoja na mabao manne katika mechi saba za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

PSG itakabiliana na AS Monaco keshokutwa ljumaa (Machi Mosi) kabla ya mechi ya mkondo wa pili ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Sociedad Machi 5, mwaka huu ambapo tayari wanafaida ya kuongoza kwa mabao 2-0.

Uwanja wa Soka Arusha kuanza kujengwa
Mada Maugo amtahadharisha Mandonga