Serikali imeanza maandalizi ya kujenga uwanja wa Soka jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2027’, ambayo yatafanyika nchini kwa ushirikiano wa Kenya na Uganda.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo, amesema serikali inaendelea na ukarabati Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujenzi wa viwanja vya kupumzikia Dodoma na Dar es salaam.
Pamoja na hayo, amesema serikali imekamilisha mkakati wa taifa wa utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Michezo ya Mwaka 1995.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, anatarajiwa kufungua mkutano wa mwaka wa wadau wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa utakaofanyika jijini Dar es Salaam Februari 29, mwaka huu ambao utahudhuriwa na watu zaidi ya 800 kutoka taasisi zinazojishughulisha na utamaduni na sanaa, kifedha, Kampuni za Bima, makampuni ya simu, vyuo vya elimu kati na juu.
Ameyataja malengo ya mkutano huo kuwa ni kuwakutanisha wadau wa utamaduni kutoka sekta binafsi na umma waweze kujenga mtandao wa kufahamiana na kujadili kwa pamoja matatizo yanayoikabili sekta hiyo pamoja na kuwatambua na kuwatunuku waliofanya vizuri kwa kuwapatia zawadi.