Mwanamasumbwi wa timu ya Taifa, Yusuph Changalawe, anatarajia kuondoka nchini leo Jumatano (Februari 28) kwenda Italia katika michuano ya mchujo, kuwania kufuzu michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Paris, Ufaransa.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza kesho Alhamis (Februari 29) hadi Machi 12, mwaka huu huku mabondia 50 wakichuana kutafuta nafasi ya kufuzu.
Akizungumzia maandalizi yake, amesema mazoezi Changalawe aliyopata yameongeza kiwango chake na yupo tayari kupambana na kutafuta nafasi ya kufuzu.
“Nakwenda katika mashindano kifua mbele, niko fiti na tayari kupeperusha bendera ya nchi yangu, naamini nitafanya vizuri na kufuzu Olimpiki,” amesema.
Mwanamasumbwi huyo amewaomba Watanzania kuendelea kumpa sapoti na kumuombea dua kwa lengo la kufanya vizuri.
“Katika mchujo uliofanyikia nchini Senegal nilifika fainali na kupata medali ya fedha, awamu hii lengo langu ni kushinda dhahabu na kufuzu, “amesema Changalawe.
Kocha wa bondia huyo, Samuel Kapungu, amesema Changalawe yupo fiti kukabiliana na wapinzani wake atakaopangiwa kuchapana nao.
“Nina imani bondia wangu atafanya vizuri kwani nidhamu, usikivu na kujituma kwake vinanipa nguvu ya kujivunia maandalizi aliyofanya,” amesema Kapungu.
Changalawe ameshawahi kushinda medali ya fedha katika mashindano ya awali ya kufuzu Olimpiki, baada ya kupoteza kwa pointi dhidi ya Abdelrahman Abdelgawwad, kutoka Misri, katika pambano lilofanyika Septemba mwaka jana, nchini Senegal.