Mlinda Lango wa Coastal Union, Ley Matampi amesema mabeki wa timu hiyo ni sababu ya yeye kufanya vizuri kutokana na hatari nyingi kuishia miguuni mwao huku akiitabiria timu hiyo nafasi nne za juu.

Matampi, raia wa DR Congo ameonekana kuwa chaguo la kocha David Ouma ambaye tangu ametua msimu huu, amecheza mechi 10 akiruhusu mabao manne tu.

Hadi sasa Matampi ndiye kinara ambaye hajaruhusu wavu wake kugusa katika mechi saba kwenye Ligi Kuu Bara akiwaacha Yona Amos (Prisons) mwenye sita, Djigui Diara wa Young Africans aliye na tano sawa na Constantine Malimi (Geita Gold) na John Noble wa Tabora United.

Matampi ambaye amewahi kuhusishwa na Simba SC na Young Africans miaka mitano iliyopita, amesema mipira ambayo muda mwingine huonekana hatari huishia miguuni mwao akieleza kuwa wametengeneza muunganiko mzuri ambao unaipa matokeo mazuri timu hiyo.

“Najivunia kiwango bora licha ya muda mfupi niliokaa Tanzania, lakini siwezi kutowapongeza mabeki kutokana na kazi nzuri wanayofanya, ipo mipira ya hatari wanaizuia.

“Hii kwangu ni mara ya kwanza kuwa kinara wa ‘Cleen Sheet’ katika Ligi Kuu, inaonyesha ubora lakini lazima niendelee kupambana na kujihakikishia nafasi zaidi kikosini,” amesema kipa huyo.

Nyota huyo wa zamani wa timu ya Taifa DR Congo, ameongeza kwamba kutokana na msimu bora alionao anatamani kwamba atabeba tuzo ya kipa bora wa Ligi Kuu na pia kuiweka timu yake nafasi ya nne.

Reliant Lusajo: Nitaibeba Mashujaa FC
Max Eberl aichimba mkwara Leverkusen