Hafla ya utoaji wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari za takwimu za Wanawake na Uongozi, zinatarajia kutafanyika siku ya Jumamosi Machi 2, 2024 Mjini Unguja.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, Dkt. Mzuri Issa imeeleza kuwa Tuzo hizo zenye kauli mbiu “Kalamu yangu, Mchango wangu kwa Wanawake” zina lengo la kuhimiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao na vyombo vya habari kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa masuala ya wanawake katika uongozi na hivyokuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali za maamuzi.

Amesema, zaidi ya washiriki 180 wanaohusika na masuala ya Habari na uongozi kutoka Unguja, Pemba na Dar Es Salaam wakiwemo Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari ambao ndio walengwa wa tuzo hizo, watashiriki katika hafla hiyo.

“Pamoja na mambo mengine, tuzo za mwaka huu zitahusisha pia mjadala mfupi wa kuangalia mafanikio na changamoto kwa waandishi wa habari na kitu gani kifanyike kuhakikisha kwamba habari za wanawake zinapaswa kupewa kipaumbele kwenyevyombo vya habari,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, kupitia taarifa hiyo Dkt. Mzuri ameeleza kuwa Tuzo hizo zimekuwa zikifanyika kwa mara ya tatu mfululizo tokea mwaka 2021, ambapo kwa mwaka huu jumla ya kazi 529 za Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya Habari Zanzibar ziliwasilishwa.

Miongoni mwa kazi hizo ni pamoja na vipindi vya radio, televisheni, makala za magazeti na zile kutoka katika mitandao ya kijamii zilizoandikwa na kurushwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuanzia mwezi Janauari hadi Desemba 31, 2023.

Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari za Takwimu za Wanawake na Uongozi zimeandaliwa kwa pamoja na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), pamoja na Jumuiya inayojihusisha na Mazingira, Usawa wa Kijinsia, na Utetezi Pemba (PEGAO), kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

Umeme: Dkt. Biteko agusia uchorongaji Visima vya Jotoardhi
Watatu wafanyiwa upandikizaji wa betri kwenye Moyo BMH