Watafiti wa Kimataifa wa Shirika la Afya Duniani – WHO, wamearifu kuwa zaidi ya watu Bilioni 1 Ulimwenguni ni wanene kupita kiasi, hali inayohusishwa na ongezeko la hatari la matatizo mengi ya kiafya.
Watafiti hao, wanasema unene uliokithiri umeenea kwa kiasi kikubwa na umekuwa jambo la kawaida kuliko kuwa na uzito mdogo katika mataifa mengi, ikiwemo nchi nyingi za kipato cha chini na cha kati, ambazo hapo awali zilikuwa zinakabiliwa na utapiamlo.
Mwandishi Mkuu wa Makala iliyochapishwa kwenye jarida la The Lancet ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Imperial cha jijini London Majid Ezzati, amesema idadi kubwa ya watu wamekuwa wakiishi na unene uliokithiri.
Hata hivyo, matokeo ambayo yanazingatiwa kati ya makadirio ya utafiti huru, yameangazia takwimu kutoka kwa zaidi ya watu milioni 220 katika zaidi ya nchi 190 Ulimwenguni kupata uhalisia wa tafiti hiyo.