Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ametangaza ratiba ya maziko ya Rais wa Mstaafu Ally Hassan Mwinyi ambaye alifariki hapo jana Febriari 29, 2024.
Ratiba hiyo, inaelekeza kuwa, leo Machi 1, 2024 majira ya saa 11:30 asubuhi mwili utaondolewa nyumbani kwa Marehemu Mikocheni kuelekea Msikiti Mkuu wa BAKWATA Kinondoni ambako Sheikh Dkt. Abubakar Bin Zuber Bin Ali ataongoza swala ya Ijumaa na taratibu zote za kidini.
Amesema, “Saa 8:00 Mchana, mwili wa utaelekea Uwanja wa Uhuru na kuanzia saa 8:30 mchana ni dua na maombi kutoka kwa Viongozi wa Dini na salamu za rambirambi kutoka kwa Viongozi mbalimbali, pia Viongozi na Wananchi mbalimbali kutoa heshima za mwisho.”
Aidha, Majaliwa amefafanua kuwa, “saa 11:00 jioni mwili utaondolewa uwanja wa Uhuru kuelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere, saa 11:30 Jioni Wananchi wa Zanzibar na maeneo mengine ya Unguja wataupokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume.”
Taarifa za kifo cha Mzee Mwinyi zilitanganzwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akilihutubia Taifa kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari.
Alisema, kifo hicho kilitokea Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es salaam, alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya Saratani ya Mapafu.
PUMZIKA KWA AMANI ALLY HASSAN MWINYI.