Baadhi ya Hospitali Binafsi zimetangaza kusitisha kutoa huduma kwa Wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya – NHIF, kutokana na kutoridhishwa na kitita kilichotangazwa na mfuko huo.

Tangazo hilo, limeainisha Vituo vilivyositisha huduma ambavyo ni Regency Medical Center, Kairuki, Hospitali za TMJ, Hospitali ya Apollo na Hospitali zote za Aga Khan nchini kuanzia Machi 1, 2024.

Kufuatia usitishwaji huo, NHIF imesema hatua hiyo ni kinyume na mkataba wa utoaji wa huduma baina yao na NHIF ambao pamoja na mambo mengine unamtaka mtoa huduma kutoa notisi ya siku 90 kabla ya kusitisha huduma.

Taarifa ya Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray iliyotolewa hii leo Machi 1, 2024 imeeleza kuwa ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza, Mfuko unawatangazia wanachama wake kutumia vituo mbadala, ili kupata huduma wanazohitaji.

Amesema, Maofisa wa NHIF watakuwa katika vituo kuhakikisha wanachama wenye changamoto wanasaidiwa kupata huduma katika vituo vingine na tayari wameshaanza kuwasiliana na wanachama wenye matibabuyanayohitaji mwendelezo wa huduma ikiwemo huduma za kuchuja damu (dialysis), ili kuwaelekeza vituo mbadala kwa ajili ya upatikanaji wa huduma hizo.

Aidha, Mziray ameeleza kuwa, tayari Mfuko unaendelea kufanya usajili wa vituo vingine binafsi, ili kuongeza wigo wa watoa huduma na kusogeza huduma kwa wanachama na kwamba wataendelea kutoa taarifa ya upatikanaji wa huduma ili kuondoa usumbufu.

Kidunda: Iwe isiwe kisasi kitalipwa
Jukumu jipya kwa Sadio Kanoute Simba SC