Chama Cha Mapinduzi – CCM, kimesema kimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wake Mstaafu na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, kilichotokea Februari 29, 2024.

Taarifa ya CCM iliyotolewa hii leo Machi 1, 2024 na Katibu Mkuu wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi imeeleza kuwa Mzee Mwinyi atakumbukwa kwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii aliyoyaongoza wakati akiwa Rais wa Tanzania (1985-1995).

Amesema, jitihada zake kubwa katika kuleta mabadiliko ya kiutendaji, kiuendeshaji na kimfumo ndani ya chama chetu alipokuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa (1990-1996) hakika hazitaachwa kukumbukwa.

Dkt.Nchimbi amesema sambamba na hayo, pia mchango wake utakumbukwa daina kwa namna alivyosaidia kujenga umoja wa kitaifa na kulinda Muungano, mojawapo ya tunu za taifa, wakati wa utumishi wake Serikalini.

Aidha, Chama Cha Mapinduzi kimesema kitaendelea kumuenzi Mzee Ali Hassan Mwinyi kwa yale yote mema aliyousia na kututendea na wanamwombea apumzike kwa amani na kuwaombea familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.

Eto’o: Song hatasaini mkataba mpya
Kidunda: Iwe isiwe kisasi kitalipwa