Kocha Mkuu Jwaneng Galaxy Morena Ramoreboli ameipiga kijembe Simba SC kuelekea mchezo wa mwisho wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24.

Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa kesho Jumamosi (Machi 02) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Kocha Ramoreboli amesema tangu walipowasili jijini Dar es salaam siku mbili zilizopita, wamekuwa wakisikia kauli mbiu ya wapinzani wao (Simba SC) kuelekea mchezo huo, ambayo inalenga kulipa kisasi ‘VITA YA KISASI’.

Kocha huyo amesema wamekuja Dar es salaam kwa lengo la kupambana na kupata matokeo, na suala la kisasi hawalipi kipaumbele, huku akiwashauri Simba SC kujipanga kulipa kisasi cha kufungwa 5-1 na Watani zao wa Jadi Young Africans.

“Nawashangaa Simba SC wametangaza kufanya kisasi na sisi Jwaneng kwanini wasifanye kisasi cha kufungwa mabao 5 kwanza waliyofungwa hapa, Sisi hatufahamu mambo ya kisasi na badala yake tumekuja kutafuta matokeo.” amesema Morena Ramoreboli

Kuelekea katika mchezo huo Simba SC kupitia Meneja wa Habari na Mawasilino Ahmed Ally alitangaza kauli mbiu ya mchezo huo ‘VITA YA KISASI’ akimaanisha wamedhamiria kulipa kisasi cha kufungwa na Jwaneng Galaxy mabao 3-1 mwaka 2021 na kutokewa katika hatua za awali katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Simba SC inahitaji ushindi wowote ili kujihakikishia kufuzu Robo Fainali, huku Jwaneng Ganaxy ikihitaji ushindi na kuiombea mabaya Wydad Casablanca itakayokuwa na mchezo dhidi ya Asec Mimosas ipoteze nyumbani kwao Morocco kutimiza malengo ya kusonga mbele.

Wydad Casablanca nayo itahitaji ushindi dhidi ya Asec Mimosas huku wakiiombea mabaya Simba SC ipoteze mchezo dhidi ya Jwaneng Galaxy, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Robo Fainali.

Pawasa: Tunautaka ubingwa COSAFA
Muhimbili kuandaa mpango wa dharura huduma NHIF