Rais wa FC Barcelona amemuomba kocha wa timu hiyo Xavi kuendelea kusalia kama Kocha Mkuu licha ya kutangaza kwamba ataondoka mwisho wa msimu.
Xavi mwenye umri wa miaka 44, alithibitisha kwamba anaondoka mwezi uliopita ambapo alisema amefanya uamuzi huo muda mrefu na kusisitiza ataondoka hata kama timu hiyo ikishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
“Hali unayojisikia ukiwa kocha wa Barcelona huwa mbaya sana, unakutana na vitendo vingi vya kukuvunjia heshima jambo ambalo linakuathiri kisaikolojia, unavumilia na mwisho unakuja kuangukia kwenye uamuzi kama huu”
Xavi alitangaza ataondoka wiki kadhaa baada ya kuibuka kwa tetesi kwamba mkurugenzi wa ufundi wa Barcelona, Deco anataka kumfukuza na kumpandisha Rafa Marquez ambaye anafundisha timu za vijana za Barca kwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Barcelona ni kwamba rais wa timu hiyo Joan Laporta hajakata tamaa juu ya Xavi na matumaini ya kwamba atamshawishi abaki kwenye timu hiyo.
Inaelezwa kwamba makamu wa rais wa Barca Rafa Yuste, amejaribu kumshawishi Xavi aendelee kuifundisha timu hiyo hadi pale mkataba wake utakapomalizika mwaka 2025.
Vigogo wanajaribu kumshawishi Xavi akubali kubakia kwa sababu wanakumbana na wakati mgumu kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya.
Inadaiwa makocha wengi wamekuwa wakikataa ofa ya Barca kwa sababu ya ukata wao wa kifedha unaowakumba kwa sasa.
Vilevile mabosi wa timu hiyo wamekuwa wakihitaji makocha wahakikishe timu inashinda mataji bila ya kuzingatia suala hilo la ufinyu wa maboresho ya kikosi.
Hata hivyo, Xavi ambaye aliiwezesha Barca kushinda taji la La Liga msimu uliopita, amekanusha taarifa za kwamba ataendelea kubaki klabuni hapo.