Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20 “Tanzanite’ imeingia kambini jana na tayari imeanza mazoezi kujiandaa na mashindano ya ‘All Africa Games’ yatakayofanyika Accra, Ghana kuanzia Machi 8 hadi 23, 2024.

Tanzanite chini chini ya Kocha Mkuu, Bakari Shime, imepangwa Kundi A ikiwa na timu za Ghana Uganda na Ethiopia.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema timu ya Tanzanite imeingia kambini kujiandaa na michuano hiyo na tayari wameanza mazoezi.

Amesema kulingana na maandalizi yanayoendelea kufanyika, TFF wana matarajio makubwa timu hiyo kufanya vizuri katika kundi lao.

“Tunaimani kubwa na kikosi cha U-20 kufanya vizuri katika michuano hiyo kwa kuwa baadhi ya wachezaji waliokuwepo kwenye timu ya Twiga Stars ndio hao wanaunda kikosi cha Tanzanite, nina uhakika uzoefu waliupata wakiwa na Twiga Stars utaisaidia timu,” amesema Ndimbo.

Amesema, TFF itaendelea kuwa karibu na timu hiyo na timu nyingine za taifa ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Kikosi cha Tanzanite kinaundwa na Golikipa Husna Mtunda (Yanga) na Washambuliaji Winifrida Gerald, Christer Bahera, Jamila Rajabu, Joyce Lema (JKT Queens), Violeth Nicholaus na Asha Mnuka (Simba), Hasnat Ubamba (Fountain Gate Princess).

Wachezaji wengine ni Zulfa Makau, Lydia Maximilian Jackline Shija na Alia Fikiri (JKT Queens), Mariamn Shaban, Ester Maseke na Jamila Selestine (Bunda Queens).

Wengine ni Sarah Joel (Fountain Gate Princess), Koku Kipanga na Zainabu Mohanmec (Simba Queens), Sabina Ales (Geita Gold Queens ), Neema Paul na Asha Omari (Yanga).

Mason Greenwood aachwa njia panda
Kapu la mabao lamfurahisha Arteta