Kiungo kutoka nchini Ufaransa, Paul Pogba ameambiwa anapaswa kuwa ‘STRONG’ baada ya kukumbana na adhabu ya kufungiwa kucheza soka kwa miaka minne.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 30 alikumbana na adhabu hiyo juzi Alhamisi baada ya kukutwa na hatia kwenye matumizi ya dawa za kusisimua misuli zinazopigwa marufuku  michezoni.

Pogba alipigwa na kukutwa ametumia virutubisho vya DHEA, ambavyo vinasisimua misuli, huku jambo hilo lilifalhamika Agosti mwaka jana na kuzuiwa kucheza mwezi uliofuata.

Adhabu ya Pogba itaanzia Septemba 11, 2023- siku ambayo alizuiwa kucheza soka baada ya kufanyiwa uchunguzi zaidi na itakwisha Septemba 10, 2027, hiyo ikiwa na maana kwamba ataruhusiwa kurudi uwanjani kipindi ambacho atakuwa ametimiza umri wa miaka 34.

Hata hivyo, katika taarifa yake aliyotoa kiungo huyo amepanga kukata rufaa kwenye Mahakama ya usuluhishi michezoni ‘CAS’ kupinga hukumu hiyo.

Pogba alisema: “Kutokana na uamuzi huu nitakata rufaa kwenye mahakama ya usuluhishi michezoni.”

Lakini, mke wa kiungo huyo wa zamani wa Manchester United, mrembo Zulay, amemtaka mumewe kuwa na moyo wa ujasiri na nguvu, alipoposti kwenye Instagram: “Ukweli wote utafahamika mfalme wangu, endelea kuwa jasiri kama ambavyo upo siku zote.”

Juventus bado haijatoa tamko lolote juu ya jambo hilo, lakini kumekuwa na madai kwamba wanajiandaa kusitisha mkataba wa kiungo huyo.

Na kutokana na mambo yalivyo kwa sasa, kiungo huyo Mfaransa anaweza kufanya uamuzi wa kustaafu soka.

Rais La Liga anamtaka Mason Greenwood
Chelsea kukwepa adhabu 2024/25