Nahodha na Mshambuliaji wa Argentina Lionel Messi amefunga bao lake la 500 la ligi wakati alipoisaidia Inter Miami kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Orlando City kwenye mchezo wa ligi ya MLS wikiendi iliyopita.
Messi aliingia uwanjani kwenye mchezo huo wa Jumamosi akiwa amefunga mabao 498 kwenye ligi baada ya kufunga bao la kusawazisha katika dakika za majerulhi kwenye sare dhidi ya LA Galaxy.
Luis Suarez aliifanya Inter Miami kuwa na mwanzo mzuri baada ya kufunga mara mbili ndani ya dakika 11 ża kwanza katika kipute hicho cha Orlando kilichofanyika kwenye Uwanja wa Chase.
Robert Taylor aliongeza bao jingine kwenye dakika 29, kabla ya Messi kufunga pale Robin Jansson aliposhindwa kuokoa mpira.
Kisha Messi alifunga kwa kichwa baada ya krosi ya Suarez kuifanya Inter Miami kushinda 5-0 na mkali huyo wa Kiargentina akifikisha bao lake la 500 kwenye ligi.
Na hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa Messi kufunga kwa kichwa tangu Mei 2021, alipofunga kipindi hicho akiwa FC Barcelona kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Celta Vigo.
Messi mwenye umri wa miaka 36, amefikisha mabao 500 ya ligi sasa, wakati mpinzani wake Cristiano Ronaldo alifikisha idadi hiyo mwaka mmoja uliopita.
Hata hivyo, Messi amefunga mara 500 kwenye mechi chache za ligi, amefanya hivyo ndani ya mechi 587, wakati Ronaldo alifunga idadi hiyo baada ya kucheza mechi 657.
Messi alifunga mabao 474 katika mechi 520 za ligi alizocheza akiwa na Barcelona kabla ya kuhamia PSG.