Lydia Mollel, Bagamoyo – Pwani.
Idadi ya Watalii wa Kigeni waliotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia na Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Machi 4, 2024 imevunjwa baada ya meli nane kutia nanga Hifadhini humo ikiwa na watalii 125 kutoka Mataifa mbalimbali na hivyo kufikisha jumla ya watalii 925 waliotembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia Februari 3, 2024.
Kwa mujibu wa takwimu za idadi ya Watalii wa kigeni waliotembelea Hifadhi hiyo katika kipindi cha hivi karibuni mwaka 2024 imetajwa kuwa ni Mwaka wenye mafanikio makubwa kwa TAWA kupata safari nyingi za meli za watalii kupitia Hifadhi hiyo.
Imeelezwa kuwa takwimu za miaka mitatu kuanzia mwaka 2022, idadi ya meli zilizotia nanga hifadhini humo zilikuwa mbili (2) zikiwa na zaidi ya Watalii 200, ambapo mwaka 2023 meli 3 ziliwasili katika Hifadhi husika zikiwa na zaidi ya watalii 300 na Mwaka huu wa 2024 meli zipatazo nane zikiwa na zaidi ya watalii 900 zimetia nanga hifadhini humo.
Ongezeko la Watalii katika Hifadhi hiyo, ni ishara kuwa utalii wa Malikale unazidi kukuwa Nchini ukichagizwa na jitihada za dhati zilizofanywa na na Serikali na sekta binafsi katika kuitangaza Nchi yetu na vivutio vyake.
Pia nguvu kubwa ya kuwekeza katika kuboresha miundombinu wezeshi ya utalii iliyofanywa na Serikali kupitia TAWA ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii wengi kutembelea hifadhi hiyo lakini bila kusahau mchango mkubwa wa Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii wa Nchi yetu.
Mapema hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Rajab Telack, aliwataka wakazi wa Wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuwa tayari kuwapokea Watalii watakaotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na kutumia fursa hiyo kufanya biashara za bidhaa za Utalii ili kujipatia kipato.