FC Barcelona imeripotiwa kuwa na mpango wa kumrudisha kocha wake wa zamani anayeinoa Paris Saint-Germain kwa sasa, Luis Enrique kurudi kupiga mzigo Camp Nou.
Mabingwa hao watetezi wa La Liga wataagana na kocha wao Xavi mwishoni mwa msimu huu baada ya kutangaza kwamba ataondoka ili aje mtu mwingine mwenye mawazo tofauti.
Xavi alibainisha hilo Januari 2024, baada ya Barca kukumbana na kichapo cha mabao 5-3 kutoka kwa Villarreal, lakini tangu wakati huo miamba hiyo haijapoteza mechi yoyote kati ya saba ilizocheza kwenye michuano yote.
Wakati ubingwa wa La Liga ukionekana kuwa mgumu kwa Barca, ambayo ipo kwenye nafasi ya tatu na imeachwa pointi nane na vinara Real Madrid, matumaini pekee ya ubingwa yapo kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano ya 16 bora dhidi ya SSC Napoli ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 ugenini huko Italia na Machi 12 watakipiga Nou Camp.
Licha ya Barca kuwa na matokeo yasiyofurahisha sana, rais wa klabu hiyo, Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo, Deco wameamua kumwacha Xavi abaki kwenye kikosi hadi mkataba wake utakapofika tamati mwishoni mwa msimu ujao.
Lakini, Xavi mwenyewe alisema ataondoka mwisho wa msimu huu.