Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania ‘TPLB’ Almasi Kasongo amesema mafanikio ya klabu za Simba SC na Young Africans kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yametokana na uwekezaji mzuri uliofanywa na timu hizo.

Miamba hiyo ya soka nchini ni miongoni mwa timu nane bora Barani Afrika zilizotinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa barani humo baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za hatua ya makundi.

Kasongo amesema uwekezaji uliofanywa na timu hizo mbili ndio msingi mkubwa wa mafanikio ya timu hizo jambo ambalo timu nyingine zinapaswa kuiga mfano huo.

“Tunajivunia mafanikio ya Simba SC na Young Africans, wameendelea kulitangaza soka la Tanzania najua lakini hiyo imetokana na uwekezaji na uaminifu wa viongozi wao ambao umeyashawishi makampuni kujitokeza kuwekeza wakiamini watapata faida,” amesema Kasongo

Kiongozi huyo amesema mbali na hilo lakini kufanya vizuri kwa timu hizo kumethibitisha maana halisi ya kazi wanayoifanya ya kuongoza mpira wa miguu nchini pamoja na kuweka taratibu na sheria na kanuni zinazouendesha mchezo huo pendwa duniani.

Kasongo amezitaka klabu nyingine kuwa na njaa ya mafanikio kama ilivyo Simba SC na Young Africans ili kupambana kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo ya kimataifa ambayo ndani yake yana faida nyingi.

Meneja wa TANROADS asimamishwa kazi
Gunia za Lumbesa zaipatia Mil. 60 Pwani