Uongozi wa Klabu ya Singida Fountain Gate umebariki kuondoka kwa aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Bruno Gomes lakini umeahidi kuisuka upya timu hiyo ili msimu ujao irudi kwenye ushindani.
Gomes amevunja mkataba kwa madai ya kukiukwa kwa baadhi ya vitu kwenye mkataba wake jambo ambalo hajapendezwa nalo.
Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, John Kadutu amesema kuna mambo mengi wamekusudia kuyafanya kwenye kikosi chao ikiwemo usajili wa nguvu ili kuiimarisha timu hiyo ilirudi katika ushindani iliyokuwa nao hapo awali.
“Unajua tangu kuanza kwa mzunguuko wa pili tumekuwa na mwenendo mbaya na hiyo imetokana na mambo mengi kutokuwa sawa ikiwemo baadhi ya wachezaji muhimu kuondoka na jana Bruno ameomba kuondoka tumeridhia,” amesema Kadutu.
Kiongozi huyo amesema mikakati yao ni kukisuka upya kikosi chao ili msimu ujao warudi kiushindani zaidi kama ilivyokuwa mwanzoni mwa msimu huu.
Singida imeendelea kuporomoka kwenye msimamo wa ligi kuu kwa sasa inashika nafasi ya nane ikiwa na alama 21 katika michezo 19 iliyocheza hadi sasa.