Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe Prince Mpumelelo Dube, amethibitisha kuondoka kwake Azam FC, baada ya kuwasilisha barua ya kuvunja mkataba na klabu hiyo ya Chamazi jijini Dar es salaam.
Dube amethibitisha kuondoka klabuni hapo baada ya kuandika waraka maalum na kuuweka katika ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram leo Alhamis (Machi 07).
Katika andiko hilo, Mshambuliaji huyo aliyedumu Azam FC kwa miaka minne, amewashukuru wachezaji wenzake na Mashabiki wa klabu hiyo iliyomsajili mwaka 2020, akitokea Highlanders FC ya nchini kwao Zimbabwe.
Dube ameandika: “Ninapoendelea na sura mpya katika kazi yangu ninabeba masomo niliyojifunza wakati nikiwa Azam FC, sapoti niliyopata kutoka kwa mashabiki ilikuwa ya ajabu. Nami nitathamini daima kumbukumbu tulizoweka pamoja.”
“Nina imani na nguvu na uwezo wa klabu hii, na sina shaka Azam FC itaendelea kufikia mambo makubwa. Nawatakia Azam FC, wachezaji wenzangu makocha na mashabiki mafanikio na furaha. Ahsante kwa safari ya ajabu.” Ameandika Dube kupitia barua yake ‘Thank You’ kwa Azam FC