Scolastica Msewa.

Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC, Kanda ya Mashariki Kusini na Kigamboni, Lillian Kapakala ameonyesha kukerwa na tabia ya baadhi ya wakazi wa maeneo ya Kigamboni na maeneo ya pembezoni mwa bahari ya Hindi kuendelea kutupa taka katika fukwe ya bahari ya Hindi na kusema tabia hiyo inaharibu mazingira na mazalia ya viumbe hai baharini.

Kapakala, ameyasema hayo katika fukwe ya Bahari ya Hindi kibugumo Kigamboni jijini Dar es salaam, wakati Wanawake wa NEMC wakifanya usafi na upandaji mikoko ikiwa maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani na kuongeza kuwa bado kumekuwa na wananchi wanaendelea kutupa taka za majumbani, maofisini na viwandani ufukweni jambo ambalo ni uchafuzi wa mazingira na kuleta athari kwa viumbe hai vingine vya bahari.

Amesema, kwenye fukwe kuna mikoko ambayo ipo kwa ajili ya kuhakikisha viumbe hai kama Samaki wanakuwa salama kwani katika usafi uliofanyika wamekuta takataka za mifuko ya plastiki, chupa za plastiki taka ambazo zinatakiwa kuyeyushwa na kutengenezwa kitu kingine lakini zimekutwa katika fukwe hiyo sehemu ambayo imetengwa kwaajili ya mazalia ya viumbe hai vya Bahari, ili waishi sehemu safi na salama wakiwa kwenye mikoko.

“Nitoe rai tu ili eneo linatakiwa kutunzwa kwa kuhakikisha takataka zote zinakwenda kwenye madampo, maeneo yaliyotengwa kwaajili ya kutupa takataka na wale wenye tabia ya kutupa takataka kwenye fukwe hizi usiku waache mara moja kwa kuzingatia Sheria za mazingira kwa kutotupa takataka fukweni” alisema Liliani.

Naye Meneja wa tafiti za mazingira wa NEMC kwaniaba ya mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Rose Mtui amesema “Miti ya mikoko ndio hutumika kuzui takataka zisiingie baharini na kuathiri viumbe hai baharini ikiwa ni pamoja na samaki, yaani mikoko ndio chujio la kuchuja takataka zisiingie baharini na zisifikie viumbe hai wetu lakini kwenye mikoko ndio sehemu ya maficho, kutagia mayai na makimbilio ya viumbe hai wakiwemo samaki hivyo ni muhimu kutunza mikoko katika fukwe zetu nchini” alisema Rose.

“Takataka za plastiki kama chuma zinavumjika vumjika na kumezwa na samaki na akishakula hutengeneza sumu katika mwili wa samaki Kisha sisi tunakula samaki hao ndipo hupelekea kupata kansa na magonjwa mbalimbali hivyo tunaona mikoko inakazi ya ziada na kubwa sana kwa mustakabali wa maisha yetu ya kila siku kwa kuchuja takataka ambazo ni sumu zote zisiingie baharini kwenye samaki wetu.” alisisitiza Mtui.

Gerard Pique: Viongozi waseme ukweli
Simba SC haijauzwa na haitauzwa