Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Tanzania imeweka sheria nyingi zinazozuia urasimu katika kupata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za kisheria.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati akifunga Mkutano wa siku tano wa Mawaziri wa Sheria kutoka katika Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola uliofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu uliofanyika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip,Uwanja wa ndege Zanzibar tarehe 8 Machi 2024.
Amewakaribisha Tanzania wawekezaji kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuchangamkia fursa za uwekezaji hususan katika uchumi wa bluu, sekta ya utalii , uwekezaji wa miundombinu, madini, kilimo, na sekta ya afya.
Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa sheria hizo zinawawezesha wananchi kupata huduma bila ya kuwepo na urasimu lakini pia zinatoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika nyanja mbalimbali bila usumbufu.
Amesema, Mifumo ya Kidigitali italeta mabadiliko makubwa katika sekta ya Sheria ambapo haki kutolewa kwa haraka kwa kuwa mashahidi hawatalazimika kufika mahakamani kutoa ushahidi, watatoa ushahidi walipo, Jaji atatoa hukumu popote alipo pia.
Rais Dkt. Mwinyi ameitaka Jumuiya ya Madola kuendelea kusimamia sheria na kuhimiza nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kuwa na sheria rafiki zinazoendana na ulimwengu wa kidijiti kwa kutoa fursa kila mtu kutambua haki zake.
Wajumbe wa Mkutano huo kutoka nchi mbalimbali walipata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii Zanzibar pia
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland KC amehudhuria mkutano huo.