Baadhi ya abiria wasio waaminifu, wanadaiwa kuwa na tabia ya kuiba vifaa hasa maboya yanayotumika wakati wa kujiokoa pindi ajali inapotokea, pindi wanaposhuka katika vivuko vya MV Kigamboni na MV Kazi.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Mhandisi Lukombe King’ombe huku akitoa onyo kwa abiria wasio waaminifu wanaotumia Vivuko hivyo kuacha mara moja tabia ya wizi.
Amesema, vitendo hivyo vinasababisha kupungua kwa maboya na hivyo kuhatarisha usalama wa abiria na mali zao, endapo itatokea dharura ya ajali.
Hayo yamejiri wakati wa zoezi maalumu la kukagua na kuhesabu idadi ya vifaa vya kujiokolea vilivyomo ndani ya vivuko vinavyotoa huduma katika eneo hilo la Magogoni lililopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.