Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola, amekataa kutupa ‘TAULO’ kwa watani wao wa jadi, Young Africans, akisema mechi bado zipo nyingi ambazo zinaweza kuwapatia ubingwa wa Tanzania Bara, huku akikiri kuna tatizo la wachezaji wake kushindwa kutumia nafasi nyingi wanazotengeneza.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara na timu yake kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union, Matola alisema pamoja na kwamba Young Africans inaendelea kufanya vema, lakini wao hawajakata tamaa kwa sababu ligi ni kama mbio ndefu, anayechanga karata zake vizuri mwishoni mwa kUmalizika ndiyo mshindi na si yule anayeongoza kwa muda mrefu.
“Siwezi kusema eti ubingwa basi kwa sababu kuna timu inafanya vizuri, sisi bado tupo kwenye mbio hizo na tuna imani tunaweza kuupata, siku zote ligi ni kama mbio ndefu, mwanariadha anaweza kuongoza kwa muda mrefu, akawa mbele kilometa nyingi, lakini zikibaki mita kadhaa watu wanapindua kibao, hii ni raundi ya 20, lakini sisi Simba SC tumecheza mechi 17, hivyo michezo mingi imebaki huwezi kututoa kwenye ubingwa,” amesema Matola.
Akiuzungumzia mchezo huo amesema ulikuwa mgumu kwa sababu nyingi, moja ni kwamba siku zote hata wakati wao wanacheza, wakikutana na Coastal Union mechi inakuwa ngumu mno, lakini kingine ni uchovu wa wachezaji.
“Niwapongeze wachezaji wetu walipambana na kutupatia pointi tatu ambazo kwa leo tulizihitaji kuliko kitu kingine chochote.
“Siku zote mechi za Simba SC na Coastal tangu sisi tunacheza zinakuwa ni ngumu, ingawa huwa tunawafunga mara kwa mara, kilichotupa ugumu mwingine ni kwamba tunacheza mechi mfululizo, wachezaji wanapata uchovu wa mwili, hii ilisababisha mechi kwetu iwe ngumu,” amesema Matola.
Amesema bado wana tatizo la kutumia nafasi wanazozipata, lakini wanashindwa kurekebisha kwa sababu ya kukosa muda.
“Ni kweli bado tuna tatizo la kutotumia nafasi, tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi, lakini tunashindwa kuzitumia, hii inasababishwa na kwamba kwa sasa tunakosa muda wa kusahihisha makosa kwenye viwanja vya mazoezi kwa kuwa kila baada ya siku mbili tunacheza mechi, lakini yote kwa yote tutarudi mazoezini na kuyafanyia kazi ili nafasi tunazozipata tuzitengeneze kuwa mabao.”
Kocha huyo pia ameonekana kufurahia kurejea Azam Complex, kwani kuna faida nyingi kwao kuliko hasara na hasa kiufundi.
Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma, amewapongeza Simba SC kwa ushindi akisema timu yake ilistahili kupoteza, hasa baada ya kukosa mabao kadhaa kabla ya wapinzani wao kupata bao la pili.
“Nafikiri ni mechi ambayo tulistahili kupoteza, nawapongeza Simba kwa kushinda mchezo huu.”
Willy Onana, alifunga bao la ushindi, ambapo kabla ya hapo, Freddy Michael alikuwa ameipatia Simba SC bao la kuongoza, kabla Lucas Kikoti kuisawazishia Coastal Union.