Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliidhinisha bajeti ya Serikali ya shilingi bilioni 44,388.1 kwa mwaka 2023/24 kutekeleza dhima ya Taifa ya kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kuhimili na kukabili athari za mabadiliko ya Tabianchi na kuimarisha sekta za uzalishaji, ili kuboresha hali ya maisha ya Wananchi.

Hayo yamesemwa hii leo Machi 11, 2024 na Waziri wa fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba Katika Mkutano wa Wabunge wa kupokea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka fedha 2024/2025, ambapo amesema Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 29,172.5 ni matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 15,215.6 ni matumizi ya maendeleo.

Amesema, “Serikali imeendelea kutekeleza dhima ya Taifa kwa kuongezea ushiriki wa sekta binafsi nchini na kuendelea kuimarisha sekta za uzalishaji zinazoajiri wananchi wengi nchini na kugharamia athari za mabadiliko ya tabia nchi zilizojitokeza.”

Hata hivyo, amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya kukumbwa na changamoto kadhaa ambazo baadhi zinatokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wa Serikali kama vile mabadiliko ya tabianchi, athari za vita na mabadiliko ya kisera za nchi zilizoendelea ikiwemo sera ya fedha ya kupunguza ukwasi katika uchumi.

“Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2023, ukuaji wa uchumi wa Taifa ulikuwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022,” amesema Nchemba.

Ameongeza kuwa, katika mwaka mzima wa 2023 Januari hadi Desemba uchumi unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji halisi wa asilimia 4.9 mwaka 2022.

Nchemba amesema mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.8 mwaka 2023 ambao ni ndani ya lengo la nchi la wastani wa kati ya asilimia 3.0 hadi 5.0 huku kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei kukitokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali.

“Na jitihada hizo ni Kuhakikisha nchi inakuwa na utoshelevu wa chakula wenye kumudu mahitaji ya soko la ndani na la nchi jirani. Kiwango cha utoshelevu wa chakula kimeongezeka kufikia asilimia 124 mwaka 2023/24 ikilinganishwa na asilimia 114 mwaka 2022/23.

“Lakini pia Kuhakikisha upatikanaji wa mbolea ambapo tani 418,942 ziliuzwa kwa wakulima kwa bei ya ruzuku katika mikoa 26 ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mbegu bora na mazao”, amesema

“Pia Kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ili kuhakikisha mazao yanasafirishwa kwa gharama nafuu kutoka maeneo ya uzalishaji vijijini hadi maeneo ya walaji, hususan masoko ya mijini na Utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti,” amesema Nchemba.

 

Ancelotti: Vinicius Jr anatendewa sivyo
Tanzania Prisons yampa jeuri Katwila