Serikali Nchini, kupitia Mfuko wa SELF (SELF Microfinance Fund), ambao upo chini ya Wizara ya Fedha umeeleza kuwa mwaka 2023 umesaidia kutengeneza ajira zaidi ya 37,024 kwa wakopaji wenyewe na wale wanaoajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini
Hayo yameezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Mudith Cheyo alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi maalum na Waandishi wa habari, Jijini Dar Es Salaam chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
SELF MF ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo hasa kwa wananchi wa kipato cha chini waweze kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato na kupunguza umasikini.
Mfuko, ulianza kutekeleza majukumu yake Julai Mwaka, 2015, ukirithi majukumu ya Mradi wa Serikali uliojulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (SELF Project) ambao ulitekelezwa kati ya mwaka 1999 hadi 2000 na mwaka 2014 hadi 2015.
“Kwa hiyo Mfuko wa SELF umesaidia kutengeza ajira kwa wakopaji kwa wao wenyewe na wale wanaoajiriwa, kiasi cha ajira 37,024 kwa mwaka 2023. Pia, kwa mwaka 2023 mfuko uliweza kutoa elimu wa fedha wa wakopaji 1,519.”
Miongoni mwa wanufaika wa mikopo kupitia mfuko huo ni Star Natural Product Ltd ambaye ni mjasiriali kwenye sekta ya viwanda vidogovidogo nchini.
Cheyo amesema, mteja huyo amekopa SELF mara tatu ambapo alianza kukopa kipindi ambacho hakuwa na sifa za kukopesheka kwenye taasisi nyingine za fedha nchini.
“Na mpaka sasa ameweza kujiendeleza na kufikia mkopo mkubwa zaidi ya shilingi milioni 100. Kutokana na uwezeshaji toka SELF ameweza kukuza karakana yake ya kutengeneza mafuta na sabuni kutokana na mchikichi.”
Pia, Afisa Mtendaji Mkuu huyo amefafanua kuwa, mjasiriamali huyo ameweza kufungua vituo viwili vya kuchaka mafuta ya mchikichi kimoja kipo Mkuranga na kingine Kibiti mkoani Pwani.
Amesema, kila kituo kimesaidia wakulima 150 katika maeneo hayo kupata huduma ya kukamua mafuta.
Mnufaika mwingine wa mikopo kupitia SELF ni Bright Future Academy ambaye ni mjasiriamali kwenye sekta ya elimu aliyeko Zanzibar.
Cheyo amesema, mteja huyo amekopa SELF mara tatu mpaka sasa na alianza kukopa SELF kipindi ambacho hakuwa na sifa za kukopesheka kwenye taasisi nyingine za fedha maka kufikia uwezo wa kukopa zaidi ya shilingi milioni 300.
“Kutokana na uwezeshaji toka SELF ameweza kutoka kwenye kupanga nyumba ya vyumba vinne, kununua kiwanja na kujenga shule yenye madarasa 32 huku akiendelea kupanua shule. Shule ya Bright Future ilikua na wanafunzi 300 na sasa wamefikia watoto 1470.”
Vile vile, Cheyo amesema kutokana na mazingira mazuri ya kusoma shule imefanikiwa kuwa shule ya kwanza Zanzibar kwa kufaulisha kwa miaka miwili kwa matokeo ya darasa la saba.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema, katika kutekeleza majukumu yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha hasa kwa wananchi wa kipato cha chini mfuko unakumbana na changamoto kadhaa.
Miongoni mwa changamoto hizo ni wananchi wengi kutokuwa na elimu ya fedha, hali inayochangia kukosa uelewa wa kutosha wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa mikopo au kutumia mikopo nje ya malengo yaliyokusudiwa.
Pia, amesema wananchi wengi hawana utamaduni wa kukopa na kurejesha, kwani utamaduni wa kurejesha mikopo kwa hiari bado ni mdogo
“Changamoto nyingine ni wananchi wengi wa kipato cha chini kujishugulisha na biashara zisizo official mfano Machinga. Hii inatoa changamoto katika kuwakopesha.”
Amesema, ili kutimiza majukumu yake kwa ufanisi mfuko umejiwekea malengo makuu matatu katika mpango mkati wake ikiwemo kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wa kipato cha chini.
Cheyo amesema, hilo litawezekana kwa kuongeza utoaji wa mikopo,kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwafikia walengwa wengi zaidi.
Jambo lingine ni kuongeza ufanisi ili kutoa huduma bora na kwa wakati. “Ili litawezekana kwa kubadilisha mifumo na kutumia zaidi teknolojia. Aidha, tuna mikakati thabiti katika uendelevu wa taasisi.”
Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema, jambo hilo linalenga kuhakikisha taasisi inajiendesha kwa faida na huduma zinazotolewa zinakuwa endelevu nchini
Hata hivyo, licha ya mfuko huu kuwa chini ya Wizara ya Fedha pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivorekebishwa.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.
Kikao kazi cha leo ni mwendelezo wa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuzikutanisha taasisi na mashirika hayo ya umma na wahariri ili ziweze kuelezea walikotoka, walipo na wanapoelekea.
Dhamira ikiwa ni ili umma ambao ndiyo wamiliki wa taasisi hizo waweze kupata mwelekeo wake na kufahamu mafanikio yao.