Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. John Jingu ametoa wito kwa wadau wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF pamoja na Kamati ya mapitio ya maboresho ya kitita cha mafao ya mwaka 2023 NHIF, Chini ya Mwenyekiti Dkt. Baghayo Saqware kupitia tena kitita kipya cha NHIF ili kuendelea kuboresha huduma za kitita katika maeneo ambayo bado yana changamoto.
Dkt. Jingu amesema hayo katika ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salama wakati wa kikao cha Kamati na APHFTA ambapo amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa kitita hicho kuna baadhi ya maeneo ambayo wadau hao wameyabainisha kama sehemu ya changamoto katika kutoa huduma.
Amesema, “ninaamini baada kuanza utekelezaji wa kitita kipya kuna maeneo tuliona yana shida lakini baada ya kuanza utekelezaji tukaona hayana shida, kwahiyo pengine sasa hivi tutakavyo kaa mezani tutaona namna gani ya kuzungumza vizuri zaidi ili kama kuna maeneo hayajakaa sawa tuyarekebishe.”
Dkt. Jingu ameongeza kuwa, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya unafanya kazi kwa ufanisi weledi na kutoa rai kwa wadau kila mmoja kuhakikisha anatoa huduma.
“Ninachotaka kuwaomba wote tujue sisi sote ni wadau wa NHIF, tunachotaka tuendelee kutoa huduma zetu vizuri na NHIF atoe huduma zake vizuri, wakati huo huo tuna kazi ya kuhakikisha tunatoa huduma bora ili tutapokuja mezani tuweze kupata maridhiano”. Amesema.