Klabu ya Azam FC imeingia makubaliano ya ushirikiano na vituo vinane vya kulea vipaji (academies) vya mikoa mbalimbali nchini Tanzania.

Vituo hivyo vinane vitafahamika kwa jina la ‘Azam FC Centers’, na vitaiwakilisha klabu hiyo ya Chamazi Dar es salaam katika mikoa husika, vikiwa na jukumu la kutafuta vipaji vya wachezaji vijana wa Kitanzania, watakajiunga na kituo cha ‘Azam FC Academy’ kutokana na mahitaji wanayoyahitaji.

Baadhi ya vituo hivyo vilivyoingia makubaliano na Azam FC ni JK7Pro Football Center (Tanga), Tutes Hub Sports Center (Songea), Maendeleo Youth Sports Center (Mtwara) na Kilwa Youth Sports Center (Lindi).

Vingine ni Muleba Youth Sports Center (Kagera), Mwanga City Sports Center (Kigoma), Rungwe Youth Sports Center (Mbeya) na Korogwe Youth Soccer Center (Korogwe).

Azam FC itavipa kipaumbele vituo hivyo katika kuvuna vipaji vya vijana, pale itakapokuwa na uhitaji wa wachezaji kwenye kituo chao cha Dar es salaam.

“Sisi kama Azam FC tunaothamini vipaji vya vijana wadogo, tutaendelea na jukumu letu la kila mara la kuvuna vipaji popote pale nchini, tukiendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika juhudi zake za kukuza maendeleo ya michezo nchini.” Imeeleza taarifa ya Azam FC

Tayari makubaliano kati ya vituo vyote hivyo na Azam FC yameingiwa kwa mikataba rasmi, zoezi likisimamiwa kwa ukaribu na Makamu Mwenyekiti, Omary Kuwe.

Mara baada ya zoezi hilo kukamilika, hivi karibuni benchi la ufundi la Azam FC  la timu za vijana, litatembelea vituo hivyo (Azam FC Centers) kwa ajili ya kukutana na makocha wanaofundisha vijana hao, lengo likiwa ni kuwajenga zaidi na kuwapa vigezo vya aina ya wachezaji wanaowahitaji.

“Kwa kuanzia, tumeanza na vituo hivyo nane, lakini katika ramani yetu tumepanga kuifikia Tanzania nzima kwa kuwa na ‘Azam Centers’ katika mikoa yote nchini.”

“Tunaamini kuwa kupitia programu hii, klabu yetu itaweza kuvuna vipaji bora vya vijana wa Kitanzania na kuviendeleza zaidi pale watakapofika kwenye kituo chetu ‘Azam FC Academy’.” Imeongeza taarifa ya Azam FC

Mama aliyeuwa Wanawe kwa Sumu Mbeya naye afariki
Tajiri Man Utd kuanza na huyu