Tanzania na Rwanda kwa pamoja zimekubaliana kuweka mazingira bora yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya Bandari ya Dar es salaam ikiwa ni moja ya njia za kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali, nchini Rwanda pamoja na waziri mwenza wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dkt. Vincent Biruta.
Rwanda imeongeza wigo wa matumizi ya Bandari ya Dar es salaam kwa zaidi ya asilimia 80 kwa usafirishaji wa mizigo yake.
Mbali na usafirishaji, Waziri Makamba na Waziri Biruta wamejadili masuala mengine ya kipaumbele kwa nchi hizi mbili kushirikiana ikiwemo Nishati, Kilimo na Teknolojia.