Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaapisha Viongozi mbalimbali (Wakuu wa Mikoa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano na Mazingira), Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka (UDART), kiapo cha maadili kwa Viongozi wa Umma.
Uapisho huo, umefamnyika Ikulu Jijini Dar es Salaam hii leo Machi 13, 2024 ambapo katika hafla hiyo amesisitiza mambo mbalimbali na hapa zipo baadhi ya nukuu muhimu.
1. “Nataka mkasimamie pia mifumo ya ukusanyaji mapato, watu wanaiba fedha watu wote mko hapo, Wakuu wa Mikoa na Wilaya mko hapo, kuna mitandao inachepusha fedha za Halmashauri huko, kuna mtandao wa Serikali na mtandao mwingine unaochepusha pesa, nashukuru Mbeya wamekuwa wa kwanza kutuambia tunafuatilia huo mtandao, na upo unaenda na wanaambizana wanachepusha pesa nyingi sana, lakini bado mnakaa huko sijui kitu gani kimeharibika mnahitaji pesa zinatoka wapi?.”
2. “Makonda amezunguka mmeona mfano wananchi wana kero kadhaa nyingine nyepesi tu za kutatuliwa kule chini lakini hawasikilizwi, na wasiposikilizwa zile ndizo kura zetu msipowasikiliza akipita mwingine akawaambia mimi nikiingia nitawasikiliza watampa, kule ndiko kuliko ushindi wa chama kilichokuwekeni vinginevyo mkifanya vingine wengine watakwenda kubeba ule ushindi waondoke nao.”
3. “Lishe ndiyo nguvu kazi tukiwa na watu goigoi nguvu kazi ya Tanzania inakwenda kuwa goigoi tukiwa na watu walioshiba vivyo hivyo, lakini hata Viongozi sisi wanaokuja nyuma yetu lazima tuwalishe vizuri, hapa pawe makini waje wajue vya kuendesha hii nchi, vinginevyo tukiwaachia hoi hoi wanakuja tu hivyo hivyo, huku wengine wanakula unga wengine wanavuta jani la Arusha, wengine hawashibi goigoi, tutakuwa na Taifa gani ndugu zangu, kwahiyo tujidhatiti kwenye lishe.”
4. “Tunashukuru sukari imesambaa na nyingine Tumeagiza sukari inakuja, nendeni mkasimamie bei na wale ambao watukutu shughulikeni nao, na niseme Odisi ya Rais TAMISEMI sasa wameanza kutathimini utendaji wa wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, Makatibu tawala na wengineo. “Kutokana na taarifa zile ndipo tunapojua nani anafanya vizuri, nani hafanyi vizuri na ndiyo maana tumefanya mabadiliko haya. Kwahiyo wakati mwingine mtu hafanyi vizuri kwa yeye mwenyewe alivyo, wakati mwingine ni mazingira yaliyopo katika eneo lake. Kwahiyo tathimini zote hizo tunazifanya.”
5. “Tunakwenda kupunguza masuala ya kukopa hasa kwa huduma za jamii sababu katika miaka mitatu hii tumekopa sana kwa ajili ya huduma za jamii, elimu, afya, maji umeme na mambo mengine, sasa tunakokwenda miaka miwili hii mnajua fika matumizi makubwa yataelekea wapi, sasa ili fedha ziweze kurudi TAMISEMI lazima tufanye jitihada za makusanyo.”